

Ndejembi ataka vijana kuandaliwa kunufaika na miradi ya mafuta, gesi
Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi ameitaka Wizara ya Nishati kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (Pura) kuandaa mpango mkakati wa kuwajengea vijana ujuzi unaohitajika katika sekta ya mafuta na gesi kabla ya kuanza kwa miradi mikubwa.
Amesema kuchelewa kuwaandaa wataalamu na watoa huduma wa ndani kunaweza kuifanya Tanzania ishindwe kunufaika na ajira na fursa za biashara zitakazotokana na uwekezaji huo.
Ndejembi amesema hayo jijini Dar es Salaam leo Jumatano, Oktoba 28, 2026, katika hafla ya utiaji saini leseni za utafutaji wa mafuta na gesi katika vitalu vya Mnazi Bay Kaskazini, West Songo Songo, Eyasi Wembere na Lindi-Mtwara.
“Tusisubiri mradi wa LNG kule Lindi ukakamilika ndiyo tuseme tunatafuta ushiriki wa wazawa, hutawapata kwa sababu itakuwa hatujawaandaa,” amesema.
Ameelekeza maandalizi yaanze kwa vijana wanaohitimu vyuo vikuu, huku kampuni za Kitanzania zikijengewa uwezo wa kusambaza bidhaa na kutoa huduma katika sekta hiyo.
Amesisitiza ushiriki wa wazawa unapaswa kuhusisha ajira, biashara na mnyororo mzima wa thamani, akionya dhidi ya kampuni za kigeni zinazojisajili nchini na kujitambulisha kama kampuni za ndani bila kuzingatia umiliki halisi.
Amesema mafanikio ya Kituo cha Ubobezi (Centre of Excellence) yatategemea maandalizi ya mapema na mifumo itakayowawezesha Watanzania kushindana kupata fursa.
Pia, amesisitiza umuhimu wa kufuatilia utekelezaji wa leseni ili miradi ikamilike kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa, akisema bila usimamizi madhubuti wananchi wanaweza kuendelea kupewa matumaini bila kuona matokeo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia mafuta na gesi, Dk James Mataragio, amesema kuipa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) leseni ya utafutaji kwa jina lake ni hatua muhimu ya kujenga uwezo wa ndani.
Amesema awali shirika hilo lilipata leseni kwa kushirikiana na kampuni za kimataifa, lakini sasa limewezeshwa kuendesha shughuli hizo kutokana na uzoefu liliojenga.
Hatua hiyo pia inalenga kuisaidia TPDC kuvutia wawekezaji wenye mitaji inayohitajika na kuongeza ushiriki wa Watanzania katika sekta hiyo.
Mataragio amesema TPDC inatarajiwa kusimamia shughuli za kitalu cha Songosongo baada ya leseni ya uendelezaji iliyokuwa ikitumiwa na kampuni ya PanAfrican kufikia ukomo. Uzalishaji katika eneo hilo ulianza mwaka 2006.
Mkurugenzi Mkuu wa TPDC, Mussa Mohamed Makame amesema katika kitalu cha Mnazi Bay Kaskazini, tafsiri ya taarifa za mitetemo za 2D na 3D imekamilika, hatua iliyosaidia kubaini maeneo yenye uwezekano wa kuwa na gesi.
Amesema hatua inayofuata ni tathmini ya kina na maandalizi ya kuchimba kisima cha kwanza cha utafutaji katika eneo la baharini lenye kina cha takribani mita 800.
Amesema katika Kitalu cha West Songo Songo, tafsiri ya taarifa za 2D imekamilika na maandalizi ya kupata mkandarasi wa kukusanya taarifa za 3D yanaendelea kabla ya uchimbaji wa kisima cha kwanza.
Amesema Kitalu cha Lindi-Mtwara kinaendelea na ukusanyaji wa taarifa za 3D, huku Eyasi Wembere ikiwa imeanza ukusanyaji wa taarifa za 2D baada ya uchunguzi wa awali wa kijiolojia na kijiokemia.
Makame amesema TPDC itazingatia ushiriki wa Watanzania na miradi ya maendeleo ya jamii katika maeneo ya shughuli hizo, akisema mafanikio ya sekta yanapaswa kupimwa pia kwa ajira, mapato na maendeleo ya wananchi.
Matumizi ya gesi yaongezeka
Waziri wa Nishati, Dk Juma Homera amesema Serikali inaendelea kupanua matumizi ya gesi asilia katika uzalishaji wa umeme, majumbani, viwandani na kwenye magari kupitia gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG).
Amesema hadi Septemba 2026, Tanzania ilikuwa na vituo 22 vya CNG, karakana 20 za kufunga mifumo ya gesi kwenye magari na zaidi ya magari 20,000 yaliyokuwa yakitumia nishati hiyo.
Aidha, amesema viwanda 37 na taasisi 31 vilikuwa vikitumia gesi asilia, huku kaya takribani 3,000 zikiwa zimeunganishiwa huduma hiyo kupitia mabomba.
Homera amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira ya kupanua matumizi ya gesi majumbani na kuongeza ushiriki wa kampuni za Kitanzania kupitia ajira, mafunzo na fursa za biashara.
Amesisitiza kuwa ushiriki wa Watanzania ni takwa la kisheria na kisera linalolenga kuhakikisha rasilimali za mafuta na gesi zinachangia ukuaji wa uchumi na kunufaisha wananchi.
You may also like

Sirro aagiza uchunguzi moto ulioteketeza vibanda 13 Kigoma

Wadau: Wazazi, walezi wawasikilize watoto badala ya kuwahukumu


Leave a Reply