

Operesheni ya Polisi Kanda ya Ziwa yanasa madereva walevi
Mwanza. Operesheni ya kushtukiza iliyofanywa usiku na Jeshi la Polisi katika mikoa mitatu ya Kanda ya Ziwa imewanasa madereva kadhaa wanaoendesha magari wakiwa wamelewa, akiwemo mmoja aliyepimwa na kukutwa na kiwango cha ulevi cha 278, huku akidai kunywa bia mbili pekee.
Operesheni hiyo iliyowakutanisha askari wa usalama barabarani kutoka mikoa ya Mwanza, Simiyu na Mara inalenga kudhibiti makosa hatarishi na kupunguza ajali zinazotokana na ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani.
Operesheni hiyo maalumu imefanyika katika Barabara Kuu ya Mwanza-Musoma, eneo la Sola, mpakani mwa mikoa ya Mwanza na Simiyu, kwa kushirikiana na Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Rorya, ambapo askari walifanya ukaguzi wa magari mbalimbali, kutoa elimu kwa madereva na abiria pamoja na kuwachukulia hatua waliobainika kukiuka sheria.
Akizungumza wakati wa operesheni hiyo, Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Mwanza, Sunday Ibrahim, amesema wamebaini makosa mbalimbali hatarishi, yakiwemo madereva kuendesha vyombo vya moto wakiwa wamelewa na kuzidisha abiria kwenye magari madogo ya usafiri aina ya Toyota Noah na Toyota Probox.
Dereva aliyeendesha gari akiwa amelewa akioneshwa matokeo ya kipimo cha kilevi na Mkuu wa Usalama barabarani Mkoa wa Mwanza, Sunday Ibrahimu ( kulia) baada ya kupimwa na kifaa cha kupimia kilichoonesha kiwango cha 278, wakati wa operesheni ya ukaguzi wa magari usiku katika eneo la Sola, barabara ya Mwanza-Musoma.
Amesema operesheni hizo zinafanyika nyakati tofauti, mchana na usiku, kwa lengo la kuhakikisha madereva wanazingatia sheria wakati wote na kwamba uwepo wa polisi barabarani si wa muda maalumu pekee.
“Baadhi ya madereva wamekuwa wakiendesha vyombo vya moto wakiwa katika hali ya ulevi. Tumewakamata na kuchukua hatua stahiki, lakini pia tumewabaini madereva wanaozidisha abiria kwenye magari aina ya Noah na Probox,” amesema Ibrahim.
Ameongeza kuwa wameendelea kutoa elimu kwa abiria kuhusu haki na wajibu wao wawapo safarini, akiwataka kutokaa kimya wanapobaini dereva anaendesha kwa mwendo usiofaa, akiwa amelewa au anakiuka taratibu nyingine za usalama.
Amesisitiza kuwa abiria wana nafasi kubwa katika kuzuia ajali kwa kutoa taarifa mapema kwa vyombo vya usalama ili hatua zichukuliwe kabla ya madhara kutokea.
Kwa upande wake, Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Mara, Adribert Ntilicha, amesema operesheni za pamoja zimeongeza mwamko wa abiria kutoa taarifa za madereva wanaokiuka sheria na kusaidia kuwabaini madereva wanaokwepa maeneo yanayofanyika ukaguzi.
“Abiria wamekuwa na mwamko wa kutoa taarifa. Hata makosa ambayo walikuwa wamezoea kuyaona yakifanywa na madereva, kwa sasa yamepungua au mengine yametoweka kabisa,” amesema Ntilicha.
Abiria wakiwa wamejazana ndani ya gari aina ya Probox, hali inayokiuka taratibu za usalama barabarani wakati wa operesheni ya ukaguzi wa magari iliyofanyika usiku katika eneo la Sola, barabara ya Mwanza-Musoma.
Katika hatua nyingine, takwimu za ukaguzi na misako ya usalama barabarani iliyofanyika katika Jiji la Mwanza kuanzia Novemba 1 hadi 17, 2026, zinaonyesha kuwa jumla ya makosa hatarishi 1,760 yamebainika na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Makosa hayo ni pamoja na ubovu wa vyombo vya moto, mwendokasi, kuyapita magari mengine katika maeneo yasiyoruhusiwa, madereva kuendesha magari wakiwa wamelewa, kuzidisha abiria, kutovaa kofia ngumu (helmet), kutoheshimu ishara na alama za barabarani pamoja na kutosimama kwenye vivuko vya watembea kwa miguu.
Katika kipindi hicho, madereva watatu wamefungiwa leseni zao za udereva kwa muda wa miezi mitatu baada ya kubainika wakiendesha magari wakiwa wamelewa.
Aidha, madereva sita wamekamatwa kwa kuendesha magari bila kuwa na leseni za udereva, huku wengine watano wakikamatwa kwa kutumia leseni zisizokuwa na sifa za kuendesha vyombo walivyokuwa wakiendesha.
Dereva wa basi, Ramadhani Ally, amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kuendesha operesheni hizo, akisema zinawasaidia madereva kuwa makini zaidi na kuzingatia sheria wanapokuwa barabarani.
“Operesheni hizi zinatusaidia sisi madereva kuwa makini na kuongeza umakini. Wakati mwingine tunapokuwa wazembe tunasahau sheria, lakini operesheni hizi zinatukumbusha wajibu wetu na kutusaidia kupunguza ajali zisizo za msingi,” amesema Ally.
Baadhi ya abiria walioshuhudia operesheni hiyo wamepongeza operesheni hiyo, wakieleza kuwa inasaidia kulinda maisha ya abiria na watumiaji wengine wa barabara.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mwanza, Sunday Ibrahim ( kulia) akitoa elimu kwa abiria kuhusu haki na wajibu wao wanapokuwa safarini, wakati wa operesheni ya ukaguzi wa magari usiku katika eneo la Sola, barabara ya Mwanza-Musoma.
Ester Sillah ameliomba Jeshi la Polisi kuendeleza ukaguzi wa mara kwa mara na kuchukua hatua kwa madereva wanaokiuka taratibu za usalama.
“Ukaguzi huu wa kushtukiza ni mzuri kwa sababu hata madereva wanaokunywa pombe kabla ya kuendesha wanakamatwa, kwani wanapokuwa wamelewa wanakuwa hawana uwezo mzuri wa kutambua hatari zilizo mbele yao,” amesema Ester.




Leave a Reply