

Polisi wawaonya wanachuo wapya dhidi ya uhalifu, dawa za kulevya
Dar es Salaam. Wanafunzi wapya wa vyuo vikuu na vyuo vya kati nchini wametakiwa kujiepusha na makundi yanayojihusisha na uhalifu, matumizi ya dawa za kulevya na vitendo vinavyoweza kuvuruga masomo yao, huku wakihimizwa kushirikiana na vyombo vya usalama kulinda maisha na mali zao.
Wito huo umetolewa na maofisa wa Jeshi la Polisi kupitia kampeni ya kutoa elimu ya ulinzi na usalama kwa wanafunzi wanaojiunga na vyuo kwa mwaka wa masomo 2026/2027, inayolenga kuwajengea uelewa wa namna ya kujilinda na kutambua vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wao.
Kupitia kampeni hiyo, Jeshi la Polisi limetembelea vyuo mbalimbali nchini, vikiwemo Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Chuo cha Ualimu Shinyanga (SHYCOM), Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT), Kampasi ya Mwanza, Chuo cha Ualimu Marangu na Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Mbalizi mkoani Mbeya.
Katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Oktoba 26, 2026, Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Magomeni, Kulwa Chupa, aliwataka wanafunzi wapya kuweka kipaumbele katika masomo na kujiepusha na makundi yanayojihusisha na vitendo visivyofaa.
“Wanachuo tunawaomba mzingatie masomo, jiepusheni na makundi yanayofanya vitendo visivyofaa, kwani lengo lenu la kuja chuoni ni kusoma na kutimiza ndoto zenu,” alisema Chupa.
Alisema wanafunzi wanaweza kushiriki katika shughuli zenye manufaa, ikiwemo michezo na shughuli za kijamii, lakini wanapaswa kuchagua makundi yanayowajenga badala ya yale yanayoweza kuwavuruga na kuwakwaza katika kufikia malengo yao.
Aliwakumbusha pia umuhimu wa kuheshimu sheria, kanuni na taratibu za vyuo, akiwataka kutoa taarifa kwa uongozi wanapobaini wenzao wanajihusisha na vitendo vinavyokwenda kinyume na taratibu hizo.
“Mkiona mwenzenu anaenda tofauti na taratibu za chuo au anajihusisha na vitendo visivyofaa, toeni taarifa kwa uongozi wa chuo ili hatua zinazostahili zichukuliwe mapema,” alisema.
Kuhusu usalama wa mali, Chupa aliwataka wanafunzi kuwa makini na maeneo wanayoishi na kutoa taarifa haraka wanapobaini matukio ya wizi au uhalifu badala ya kukaa kimya.
Aliwahimiza pia kuchukua tahadhari dhidi ya majanga ya moto kwa kuzima vifaa vya umeme na vyanzo vingine vya moto wanapokuwa hawavitumii, ili kuzuia ajali zinazoweza kuhatarisha maisha na mali zao.
Akizungumza na Mwananchi Novemba 1, 2026, Chupa amesema elimu hiyo inalenga kuwakumbusha wanafunzi umuhimu wa kuzingatia maadili na kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi pamoja na zile zinazosimamia taasisi zao za elimu.
Amesema wanatarajia elimu hiyo itawasaidia wanafunzi kuelewa wajibu wao wanapokuwa chuoni na kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wao na wa wengine, huku wakizingatia lengo lao kuu la kujiunga na vyuo, ambalo ni kupata elimu na kutimiza ndoto zao.
Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Samweli Kijanga,akitoa elimu ya uzalendo kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Jordan cha Morogoro Oktoba 30, 2026, na akiwahimiza kuzingatia tunu za taifa, kulinda amani na kudumisha umoja na mshikamano kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
Dawa za kulevya, mitandao
Kwa upande wa Shinyanga, Oktoba 27, 2026, Jeshi la Polisi lilitoa elimu hiyo kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo cha Ualimu Shinyanga (SHYCOM), likisisitiza umuhimu wa kujiepusha na uhalifu, matumizi ya dawa za kulevya, ulevi na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.
Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Shinyanga, Fraterian Tesha, aliwataka wanafunzi kuzingatia maadili na kutambua wajibu wao katika kulinda usalama wao na wa wenzao wanapokuwa chuoni.
Wakati huohuo, Oktoba 31, 2026, wanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo cha Ualimu Marangu (TTC), mkoani Kilimanjaro, walitakiwa kuzingatia masomo, kujiepusha na makundi yanayoweza kuwashawishi kujiingiza katika uhalifu na kuwa wazalendo kwa kulinda amani ya nchi.
Wito huo ulitolewa na Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Kilimanjaro, Lazaro Mwanyasi, wakati akitoa elimu kwa wanafunzi hao kupitia kampeni ya Ongea na Kamanda iliyofanyika katika ukumbi mdogo wa mikutano wa chuo hicho.
“Wanafunzi tumieni vizuri fursa ya elimu mliyoipata, kuheshimu sheria na kanuni za chuo, kuepuka kufuata mkumbo na kutoshiriki vitendo vinavyoweza kuvuruga amani na usalama wa nchi,” alisema Mwanyasi.
Aliwahimiza wanafunzi kutoa taarifa kwa wakati kuhusu uhalifu na watu wanaojihusisha na vitendo hivyo, akieleza kuwa ushirikiano kati ya wananchi na Jeshi la Polisi ni msingi muhimu katika kuzuia na kupambana na uhalifu.
Wakumbushwa kujiepusha na ukatili
Katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT), Kampasi ya Mwanza, Oktoba 28, 2026, Jeshi la Polisi lilitoa elimu kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza kuhusu ulinzi na usalama, likiwataka kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha maisha yao na kuvuruga masomo.
Mkuu wa Dawati la Jinsia na Ulinzi wa Mtoto Mkoa wa Mwanza, Faraja Mkinga, alisisitiza umuhimu wa wanafunzi kujiepusha na ukatili na unyanyasaji, huku wakitumia muda wao katika shughuli za kitaaluma na zenye tija.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga, alitoa elimu kuhusu usalama na matumizi ya mitandao ya kijamii kwa wanafunzi wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Mbalizi, Oktoba 28, 2026.
Kuzaga aliwataka wanafunzi kuwa makini wanapotumia mitandao ya kijamii na kuepuka kusambaza taarifa zinazoweza kuwaingiza katika matatizo ya kisheria.
You may also like

Chadema yaweka masharti kushiriki maridhiano

6,800 Lindi residents to gain better connectivity


Leave a Reply