

Rais Samia apongezwa kufanikisha mkutano wa IPU Arusha
Dodoma. Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (CCM) amewasilisha bungeni azimio la kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake katika kufanikisha Mkutano Mkuu wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), uliofanyika Arusha Oktoba 5 hadi 9, 2026.
Akiwasilisha azimio hilo leo Jumanne Oktoba 27, 2026, Nape amesema mkutano huo haukuwa tukio la kawaida la kimataifa, bali ulikuwa wa kihistoria kwa Tanzania, uliothibitisha nafasi ya nchi katika diplomasia ya mabunge na kuimarisha uwakilishi wa Afrika katika uongozi wa taasisi za kimataifa.
“Uamuzi wa IPU kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huu ni matokeo ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha utawala bora na diplomasia ya nchi katika medani za kimataifa,” amesema Nape.
Nape amesema kujenga nchi si kazi rahisi, akiwataka Watanzania kutoruhusu watu wachache wasiolitakia mema Taifa kuandika historia yake kwa mtazamo usioakisi mazuri yaliyofanyika.
Amesisitiza kuwa Watanzania wanapaswa kujivunia nchi yao na kutembea kifua mbele pamoja na Rais Samia, akisema amefanikiwa katika juhudi za kuiwakilisha Tanzania kimataifa.
Mkutano huo uliofanyika Arusha ulikuwa na lengo la kumchagua Rais wa 32 wa IPU baada ya Spika wa zamani wa Tanzania, Dk Tulia Ackson, kumaliza muda wake kama Rais wa 31 wa umoja huo.
Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano huo kwa mara ya kwanza tangu IPU ilipoanzishwa mwaka 1889.
Pia, ilikuwa mara ya kwanza kwa Mtanzania kushika nafasi ya urais wa umoja huo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizowasilishwa na Nape, zaidi ya washiriki 2,000 walihudhuria mkutano huo, wakiwamo maspika 56 na naibu spika 51, pamoja na maofisa wengine.
Mkutano huo ulifanyika chini ya kaulimbiu ya kuimarisha utawala bora na kuwezesha jamii kupitia ushirikishwaji, uaminifu na fursa kwa wote.
Nape amesema mkutano huo pia umeweka alama katika ushiriki wa wanawake, waliokuwa asilimia 39.4 ya wabunge waliohudhuria.
Amesema hatua hiyo, ikiunganishwa na historia ya uongozi wa Dk Tulia Ackson, inasisitiza umuhimu wa kuendelea kuongeza nafasi za wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika uongozi na maamuzi.
Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe amesema mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha Rais Samia yanaimarisha nafasi ya Tanzania kimataifa.
Bashe amesema Rais Samia amekuwa akishiriki katika kampeni za Watanzania wanaowania nafasi mbalimbali katika taasisi za kimataifa, akitolea mfano jitihada alizofanya wakati Dk Tulia Ackson alipowania urais wa IPU.
“Miaka michache iliyopita wakati Dk Tulia Ackson (Spika mstaafu) alipogombea nafasi ya Rais wa IPU, Marehemu Dk Faustine Ndugulile na Profesa Janabi maeneo yote Rais alikuwa anapiga simu kwa viongozi wenzake kufanya kampeni, kwa hili lazima tupongeze,” amesema Bashe.
Mbunge wa Kisarawe, Dk Seleman Jafo amesema Watanzania wamepata heshima kutokana na kiongozi wa Bunge lao kupewa nafasi ya kuongoza mkutano huo, akihusisha mafanikio hayo na uongozi wa Rais Samia.
Mbunge wa Arusha Mjini, Paul Makonda amesema mkutano huo umeutangaza mji wa Arusha kimataifa, akiiomba Serikali kuendelea kupeleka mikutano mikubwa ya kimataifa katika jiji hilo.
Naye Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya amesema baadhi ya watu waliwahi kuibeza Tanzania, lakini mafanikio ya kidiplomasia yameonesha nafasi ya nchi katika medani za kimataifa.
Spika wa Bunge, Mussa Zungu, amesema wakati wa maandalizi ya mkutano huo, walikuwa na lengo la kuonesha kwa dunia maendeleo yaliyofikiwa na Tanzania.
Amesema washiriki walipowasili walipata fursa ya kujionea maendeleo katika sekta mbalimbali, zikiwamo afya, maji, umeme na miundombinu.
Akizungumzia hotuba ya Rais Samia iliyosomwa na Waziri Mkuu, Zungu amesema washiriki walivutiwa na maendeleo yaliyofikiwa na Tanzania pamoja na msimamo wake wa kudumisha uhusiano mwema na mataifa mengine.
Amesema katika mazungumzo na washiriki, masuala ya maendeleo na uwekezaji yalikuwa miongoni mwa yaliyopewa kipaumbele, akisisitiza kuwa Tanzania haina ugomvi na nchi yoyote na inachukulia mataifa mengine kuwa marafiki.
Hata hivyo, Zungu amesema ujenzi wa Taifa hauwezi kufanywa na chama kimoja pekee, akivitaka vyama na makundi mengine kurejea mezani na kushirikiana katika kujadili masuala ya maendeleo.
You may also like

Chadema, Magereza zatofautiana kuhusu mgomo wa kula kwa Lissu

Polisi Dodoma yawahakikishia usalama wanaofanya biashara usiku


Leave a Reply