

Samia agawa wizara, ateua mawaziri wapya
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri kwa kugawa wizara mbili na kuunda wizara nne, hatua iliyoambatana na uteuzi wa mawaziri, makatibu wakuu na viongozi wengine waandamizi wa Serikali.
Katika mabadiliko hayo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imegawanywa na kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Vilevile, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imegawanywa na kuunda Wizara ya Mifugo na Wizara ya Uvuvi.
Aidha, Rais Samia amefanya mabadiliko kwa Msemaji Mkuu wa Serikali kwa kumteua Dk Ayub Rioba.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi usiku wa leo Jumatano, Novemba 25, 2026 na Dk Moses Kusiluka, mabadiliko hayo yamefanyika sambamba na uteuzi na uhamisho wa viongozi mbalimbali wa Serikali kwa lengo la kuimarisha utendaji.
Katika uteuzi wa mawaziri, Balozi Mahmoud Thabit Kombo ameendelea kuongoza sekta ya mambo ya nje baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, huku Angellah Kairuki akiteuliwa kuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Kairuki anahamia katika wizara hiyo akitokea Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, ambako nafasi yake imechukuliwa na Beng’i Mazana Issa aliyeteuliwa kuwa waziri wa wizara hiyo.
Katika wizara zilizogawanywa, Dk Bashiru Ally ameteuliwa kuwa Waziri wa Mifugo, huku Hamis Mwinjuma, maarufu Mwana FA akipewa dhamana ya kuongoza Wizara ya Uvuvi.
Kabla ya uteuzi huo, Mwana FA alikuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Sasa atakuwa miongoni mwa viongozi watakaosimamia sekta ya uvuvi kupitia wizara inayojitegemea.
Mabadiliko mengine ni uteuzi wa David Silinde kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Kabla ya uteuzi huo, Silinde alikuwa Naibu Waziri wa Kilimo. Anakwenda kuchukua nafasi ya Dk Leonard Akwiapo ambaye amewekwa kando.
Katika nafasi za naibu mawaziri, Dk Ngwaru Maghembe ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, huku James Millya akipewa nafasi hiyo katika Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Ng’wasi Kamani ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mifugo. Subira Mgalu
ambaye amewahi kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini amerejea tena sasa atakuwa Naibu Waziri wa Uvuvi.
Aidha, Rais Samia amemteua Mwenyekiti wa Bunge, Cecilia Paresso kuwa Naibu Waziri wa Kilimo.
Mabadiliko makatibu wakuu
Katika ngazi ya makatibu wakuu, Rais Samia amefanya mabadiliko yaliyohusisha wizara mpya na ofisi mbalimbali za Serikali.
Agnes Meena ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo, huku Profesa Mohammed Ali Sheikh akiteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uvuvi.
Eliakim Maswi amehamishwa kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu na kupangiwa kuwa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Naye Gerson Msigwa amehamishwa kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na kupangiwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu.
Abdallah Mitawi ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, akitokea nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi.
Katika sekta ya mambo ya nje, Balozi Samwel Shelukindo amepangiwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, huku Charles Kadonya akiteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Katika nafasi za naibu makatibu wakuu, Balozi Said Shaib Mussa amepangiwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, huku Dk Fabian Madele akipangiwa nafasi hiyo katika Wizara ya Mifugo.
Dadi Kolimba ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uvuvi, akitokea nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara-Mikindani.
Mabadiliko mengine ni uhamisho wa Elijah Mwandumbya kutoka Wizara ya Fedha kwenda Wizara ya Uchukuzi, ambako atakuwa Naibu Katibu Mkuu.
Dk Amos Ibrahim ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha anayeshughulikia masuala ya usimamizi wa uchumi. Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo cha Kodi.
Katika uteuzi mwingine, Dk Ayub Rioba ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali.
Dk Rioba amewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC). Amechukua nafasi iliyoachwa wazi na Gerson Msigwa.
Aidha, Balozi Meja Jenerali Wilbert Ibuge amepangiwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Brazil, akitokea nafasi ya Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi.
Katika sekta ya miundombinu, Mhandisi Gilbert Mwoga ameteuliwa kuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), akichukua nafasi ya Mhandisi Victor Hudson Seff aliyemaliza muda wake.
Kabla ya uteuzi huo, Mwoga alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Miundombinu katika Ofisi ya Waziri Mkuu-Tamisemi.
Pia, Katibu Mkuu Mstaafu, Adolf Ndunguru, ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), akichukua nafasi ya Zakhia Hamani Meghji aliyemaliza muda wake.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uapisho wa mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu wateule utafanyika katika tarehe itakayopangwa baadaye.
You may also like

Aibu! Mbunge anaswa na CCTV akiweka simu ya mwenzake mfukoni

Wadau wa maendeleo waunga mkono Sifuri Tatu ya Samia


Leave a Reply