

Aibu! Mbunge anaswa na CCTV akiweka simu ya mwenzake mfukoni
Moshi/Nairobi. Spika wa Bunge la Kenya, Moses Wetang’ula, amefichua kuwa kamera za usalama (CCTV) zilimnasa mbunge mmoja wa kiume akichukua simu ya mkononi ya mbunge mwenzake na kuiweka mfukoni, katika tukio lililotokea ndani ya ukumbi wa Bunge.
Wetang’ula amesema picha hizo zinaonyesha mbunge huyo akichukua simu hiyo kutoka kwenye kiti baada ya kutokea vurugu, kisha kuiweka mfukoni mwa suruali yake.
Akizungumza bungeni leo, Novemba 25, 2026, Spika huyo amefafanua kauli yake ya awali aliyotoa Novemba 24, akisisitiza kuwa hakumtaja mbunge huyo kwa jina wala hakumtuhumu rasmi kwa wizi.
Amesema kumbukumbu rasmi za shughuli za Bunge (Hansard) zitaonyesha maneno halisi aliyotumia katika maelezo yake ya awali, akifafanua kuwa hakutumia neno ‘kuiba’ kumwelezea mbunge huyo.
‘NO HONOR among thieves… ‘ An MP captured on camera ‘stealing’ a colleague’s mobile phone inside Kenya’s National Assembly. https://t.co/m5jtWICPRB
— Linus Kaikai (@LinusKaikai) November 25, 2026
Ufafanuzi huo umetolewa baada ya Mbunge wa Kuteuliwa, Sabina Chege, kuzungumzia kupotea kwa simu yake wakati wa vurugu zilizotokea Juni 8, 2023.
Chege alimtaka Spika kumtaja mtu aliyeonekana kwenye kamera akichukua simu hiyo au kuhakikisha inarejeshwa kabla ya kumalizika kwa muhula wa sasa wa Bunge.
Akijibu hoja hiyo, Wetang’ula amesema picha za CCTV zililetwa ofisini kwake na kutazamwa pamoja na Kiongozi wa Wengi na baadhi ya wabunge wengine.
Amesema walimuona mbunge mmoja wa kiume akichukua simu kutoka kwenye kiti cha mbunge mwingine na kuiweka mfukoni.
“Kamera za CCTV zikaletwa ofisini kwangu. Tulizitazama pamoja na Kiongozi wa Wengi na wabunge wengine mmoja au wawili, na kwa hakika tulimuona mbunge mmoja akiweka simu ya mbunge mwingine mfukoni mwake,” amesema.
“That phone was just one week old,” Sabina Chege narrates how she lost her iPhone 16 in Parliament, claiming it was stolen by a fellow MP! https://t.co/EXvzRzTkiU
— The Kenyan Vigilante (@KenyanSays) November 25, 2026
Ameongeza kuwa mbunge huyo aliitwa na kuonyeshwa picha hizo, lakini alikanusha kuchukua simu hiyo licha ya kuonekana kwenye video akiichukua na kuiweka mfukoni.
Wetang’ula amesema aliamua kutomtaja hadharani mbunge huyo, badala yake akamwachia suala hilo ajitathmini mwenyewe.
“Nilimwambia aende akapambane na dhamira yake kwa kipindi chote kilichosalia cha muhula huu, kwa sababu kuna mambo fulani ambayo hayatarajiwi kutoka kwetu (wabunge),” amesema.
Hata hivyo, Spika huyo ameagiza picha za CCTV zinazohusiana na tukio hilo ziwasilishwe kwenye Kamati ya Bunge ya Haki na Madaraka ya Bunge kwa ajili ya kushughulikiwa.
Amesema hatakuwa mwenyekiti wa kamati hiyo, bali atamteua mtu mwingine kuisimamia ili kuondoa uwezekano wa mgongano wa masilahi katika kushughulikia suala hilo.
“Stop being a crybaby Sabina.” Drama as Millie Odhiambo clashes with Sabina Chege in parliament after Sabina Chege exposes that it was her phone that was stolen from Parliament by a fellow MP. https://t.co/3bdvV0quss
— The Reporter Ke (@Kethereporter) November 25, 2026
Wetang’ula pia ametumia tukio hilo kuwakumbusha wabunge umuhimu wa kuzingatia maadili na kulinda imani ya wananchi kwa viongozi waliowachagua kuwawakilisha.
Wakati suala hilo likiendelea kujadiliwa, Mbunge wa Mumias Mashariki, Peter Salasya, amemtetea mbunge anayetajwa kwenye tukio hilo, akitoa uwezekano kuwa huenda alichukua simu hiyo akidhani ni yake kwa kuwa simu nyingi zinafanana.
Salasya amedai kuwa mbunge anayepokea mshahara wa zaidi ya Sh1 milioni za Kenya hawezi kuiba simu yenye thamani ya Sh100,000 za Kenya.
Amesema kuweka tukio hilo wazi kwa umma kunaweza kuathiri taswira ya Bunge.
Tangu maelezo ya Spika yalipoanza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, mjadala kuhusu tukio hilo umeongezeka, huku baadhi ya watumiaji wa mitandao hiyo wakianza kutaja majina ya wabunge wanaodhaniwa kuhusika.
You may also like

Samia agawa wizara, ateua mawaziri wapya

Wadau wa maendeleo waunga mkono Sifuri Tatu ya Samia


Leave a Reply