

Hivi ndivyo MMama inavyookoa maisha ya wajawazito
Dar es Salaam. Simu inapopigwa usiku wa manane kutoka kijijini kumjulisha mama mjamzito anahitaji huduma ya dharura, kila dakika inayopita inaweza kuwa tofauti kati ya uhai na kifo.
Hapo ndipo umuhimu wa mpango wa usafiri wa dharura kwa wajawazito na watoto wachanga (MMama) unapojidhihirisha.
Kupitia mfumo huo, zaidi ya rufaa 100,000 zimeratibiwa tangu mwaka 2025, hatua inayodhihirisha mchango wake katika kuunganisha wajawazito na watoto wachanga wanaohitaji huduma za haraka na vituo vinavyoweza kuwahudumia.
Vifo vya wajawazito nchini vimeendelea kupungua kutoka 104 mwaka 2022 hadi takribani 75 mwaka 2026 kwa kila vizazi hai 100,000, kwa mujibu wa takwimu mpya zinazotarajiwa kuzinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kesho, Novemba 26, 2026.
Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, Serikali inataka ushahidi wa kisayansi kubaini kama mfumo huo unaendelea kufanya kazi kwa ufanisi katika maeneo yote, hususan vijijini ambako umbali, upatikanaji wa magari na changamoto za miundombinu vinaweza kuchelewesha huduma.
Akifungua Mkutano wa Tatu wa Kitaifa wa Kisayansi kuhusu Afya ya Uzazi, Mama, Mtoto Mchanga, Mtoto, Vijana na Lishe (RMNCAH+N), jijini Dar es Salaam leo Jumatano, Novemba 25, 2026 Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Bruno Sunguya, amesema takwimu za kitaifa pekee haziwezi kueleza kikamilifu hali halisi ya huduma katika maeneo ya wananchi.
Amesema pamoja na dashibodi kuonyesha idadi ya rufaa zilizoratibiwa, ni muhimu kujua kama huduma zinapatikana kwa wakati, magari yako tayari wakati wa dharura na madereva wanawezeshwa kutekeleza majukumu yao.
“Dashibodi zinatuonyesha kile kilichoripotiwa, lakini je, taarifa hizo zinaeleza kile kinachotokea katika maeneo ya huduma, vituo vya kuratibu rufaa na vijijini wakati wa usiku?” Amehoji.
Profesa Sunguya ametaja changamoto za kucheleweshewa malipo madereva wanaoshiriki katika mfumo huo, upatikanaji wa magari ya dharura na uwajibikaji wa wahusika kuwa miongoni mwa maeneo yanayohitaji kuchunguzwa.
Amesema tathmini hiyo itasaidia Serikali kutambua mafanikio yaliyopatikana, mapungufu yaliyopo na hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kuufanya mfumo huo kuwa endelevu.
Kwa mujibu wake, MMama ulianza mwaka 2013 kama jaribio katika maeneo ya Singida, ukiwa na lengo la kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga.
Katika hatua za awali, ulijumuisha ujenzi wa nyumba za kusubiria kujifungua karibu na vituo vya afya na mfumo wa rufaa uliotumia usafiri wa umma kwa kushirikisha madereva wa jamii.
Kati ya mwaka 2017 na 2021, mpango huo ulipanuliwa katika Mkoa wa Shinyanga, ambako tathmini na tafiti za kisayansi zilisaidia kutoa ushahidi wa ufanisi wake.
Aprili 2022, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ulizinduliwa kwa ajili ya kupanuliwa nchini kote. Kufikia Oktoba 2023, ulikuwa umefikia mikoa yote 31 ya Tanzania Bara na Zanzibar, kabla ya kuingizwa katika mfumo wa kitaifa wa huduma za dharura za afya Mei 2025.
Profesa Sunguya amesema Serikali sasa inaendelea kuimarisha umiliki wa mpango huo kwa kuhamishia mifumo yake ya kidijitali katika majukwaa ya Serikali na kuhusisha timu za afya za mikoa na halmashauri katika usimamizi.
Ameongeza kuwa baadhi ya halmashauri zimeanza kutenga fedha za kuwalipa madereva wanaoshiriki kutoa huduma hizo kupitia mipango yao ya mwaka ya afya.
Tathmini iliyowasilishwa katika mkutano huo imehusisha maswali 27 katika maeneo tisa ya uchunguzi, majadiliano 69 ya vikundi na ukusanyaji wa taarifa katika maeneo ya Singida, Manyara, Rukwa na Zanzibar.
Mhudumu wa kituo cha kuratibu huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tumbi, Delila Siigwa, amesema jukumu lao si kupokea simu za dharura pekee, bali kuhakikisha mgonjwa anafikishwa katika kituo chenye uwezo wa kumpatia huduma inayohitajika.
Amesema baada ya kupokea taarifa, huwasiliana na kituo husika ili kuhakikisha maandalizi ya kumpokea mgonjwa yanafanyika kabla ya kuwasili kwake.
Pia, wanafuatilia safari ya mgonjwa na kuhifadhi taarifa muhimu huku wakiratibu mawasiliano kati ya wahusika ili kuzuia ucheleweshaji.
Kwa upande wake, dereva wa ambulensi, Sale Maziku, amesema jukumu la madereva ni kuhakikisha wagonjwa wanachukuliwa kwa wakati na kufikishwa katika vituo vilivyopangwa, huku wakiendelea kutoa taarifa kwa kituo cha uratibu kuhusu safari.
Mkutano huo wa RMNCAH+N unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, unaendelea hadi Novemba 27, 2026.
Katika siku yake ya kwanza, mijadala ilijikita pia katika afya ya watoto wachanga, ikiwamo hatua za kuboresha huduma wanazopata tangu kuzaliwa.
Kupitia kaulimbiu yake inayosisitiza upatikanaji wa huduma bora na zenye usawa kwa ufadhili endelevu, ubunifu na mifumo imara ya afya, mkutano huo unalenga kuweka mikakati ya kuimarisha huduma za mama, mtoto, vijana na lishe
You may also like

Samia agawa wizara, ateua mawaziri wapya

Aibu! Mbunge anaswa na CCTV akiweka simu ya mwenzake mfukoni


Leave a Reply