

Wadau wa maendeleo waunga mkono Sifuri Tatu ya Samia
Dar es Salaam. Wadau wa maendeleo wa sekta ya afya wameonesha utayari wa kushirikiana na nchi za Afrika katika kutekeleza Ajenda ya Sifuri Tatu ya Rais Samia Suluhu Hassan, inayolenga kumaliza vifo vinavyoweza kuzuilika vya mama na watoto wachanga, uzazi wa nyumbani na watoto kukosa chanjo.
Ahadi hiyo imetolewa Novemba 25, 2026, jijini Addis Ababa, Ethiopia, katika mkutano wa ngazi ya juu uliojadili utekelezaji wa Mpango Elekezi wa Afya ya Uzazi, Mama, Mtoto Mchanga, Watoto na Vijana (RMNCAH) wa Umoja wa Afrika wa mwaka 2026–2030.
Mkutano huo umefanyika siku moja baada ya Rais Samia, ambaye ni Kinara wa Umoja wa Afrika wa Masuala ya Afya ya Mama na Mtoto, kuzindua rasmi mpango huo wakati wa Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Afrika (CPHIA 2026).
Wawakilishi wa mashirika na taasisi mbalimbali za maendeleo wameeleza utayari wa kuunganisha nguvu na Serikali za Afrika ili kuongeza uwekezaji, kuimarisha huduma za afya na kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanatekelezwa.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Sekretarieti ya Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Mama na Mtoto, Ummy Mwalimu, amesema hatua inayofuata ni kuhakikisha dhamira ya kisiasa iliyooneshwa kupitia mpango huo inabadilika kuwa uwekezaji na utekelezaji wenye matokeo.
Amesema sekretarieti itaendelea kushirikiana na viongozi wa Afrika, kuratibu mikutano ya kitaalamu, kuhamasisha upatikanaji wa fedha na kuimarisha mifumo ya uwajibikaji ili nchi wanachama zitimize ahadi zao.
Mkuu wa Sekretarieti ya Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Mama na Mtoto, Ummy Mwalimu akizungumza leo Jumatano, Novemba 25, 2026 wakati wa mkutano wa ngazi ya juu uliojadili utekelezaji wa Mpango Elekezi wa Afya ya Uzazi, mama na mtoto mchanga
“Sekretarieti itaendeleza ushawishi kwa viongozi wa Afrika, kuratibu mikutano ya kitaalamu, kuhamasisha rasilimali za kifedha na kuimarisha mifumo ya uwajibikaji ili kuhakikisha nchi zinatimiza ahadi zilizowekwa,” amesema.
Miongoni mwa taasisi na mashirika yaliyoonesha utayari wa kushirikiana ni Mohammed Bin Zayed Foundation for Humanity, Gates Foundation, Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), Beginnings Fund, Pathfinder, Laerdal Global Health, Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA-HC), pamoja na Serikali ya Norway.
Wawakilishi wake ni pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Mohammed Bin Zayed Foundation for Humanity, Dk Shamma Khalifa Al Mazrouei, Afisa Programu Mwandamizi wa Gates Foundation, Samwel Mulyanga na Mkurugenzi wa Kanda wa UNFPA Afrika Magharibi na Kati, Dk Sennen Hounton.
Wengine ni Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa Pathfinder, Dk Tabinda Sarosh, Mkurugenzi Mtendaji wa Laerdal Global Health, Karoline Myklebust na Mkurugenzi Mkuu wa ECSA-HC, Dk Ntuli Kapologwe.
Utayari huo unakuja wakati Afrika ikiendelea kukabiliwa na mzigo mkubwa wa vifo vya wajawazito na watoto, hali inayotaka hatua za haraka katika kuimarisha mifumo ya afya.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (Africa CDC), Profesa Diana Nambatya Nsubuga, amesema asilimia 70 ya vifo vya wajawazito duniani hutokea Afrika, huku bara hilo likichangia asilimia 58 ya vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano.
Amesema takwimu hizo zinaonesha umuhimu wa kuongeza kasi ya utekelezaji wa afua za afya zenye matokeo makubwa, ili kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika na kuhakikisha watoto wote wanapata huduma muhimu za chanjo.
Kwa upande wake, Mshauri wa Kiufundi wa Sekretarieti ya Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Mama na Mtoto, Dk Sunday Dominico, amesema utekelezaji wa malengo hayo unahitaji mifumo ya afya yenye uwezo wa kutoa huduma bora.
Amesema kumaliza uzazi wa nyumbani kunahitaji vituo vya afya kuwa na watumishi wenye ujuzi, vifaa tiba na uwezo wa kutoa huduma za dharura na rufaa kwa wajawazito na watoto wachanga.
Ameongeza kuwa kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika kunahitaji uchunguzi wa kina wa kila kifo na ufuatiliaji wa utekelezaji wa mapendekezo ya wataalamu, huku kuondoa watoto wanaokosa chanjo kukihitaji kuimarisha huduma hizo na kuwafikia wote.
Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Nassoro Mazrui, akizungumza leo Jumatano, Novemba 25, 2026 wakati wa mkutano wa ngazi ya juu uliojadili utekelezaji wa Mpango Elekezi wa Afya ya Uzazi, mama na mtoto mchanga
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Nassoro Mazrui, amesema uzoefu wa Tanzania unaonesha kuwa uongozi na uwekezaji endelevu katika sekta ya afya unaweza kuchangia kupunguza vifo vya mama na kuboresha huduma.
Amesema takwimu za tafiti za afya na demografia zinaonesha vifo vya wajawazito nchini vilipungua kutoka 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000 kati ya mwaka 2015/16 na 2022, huku asilimia 80 ya wanawake wakijifungulia katika vituo vya afya mwaka 2022.
Ameongeza kuwa matokeo ya awali ya utafiti mpya wa kitaifa yanaonesha kupungua zaidi kwa vifo hivyo, hatua inayokaribia lengo la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) la kufikia vifo visivyozidi 70 kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2030.
Kupitia mpango huo, Umoja wa Afrika na wadau wa maendeleo wanalenga kuimarisha ushirikiano, uwekezaji na uwajibikaji ili kuhakikisha wanawake wanapata huduma salama wakati wa ujauzito na kujifungua, huku watoto wakipata huduma muhimu za afya tangu wanapozaliwa.
You may also like

Samia agawa wizara, ateua mawaziri wapya

Aibu! Mbunge anaswa na CCTV akiweka simu ya mwenzake mfukoni


Leave a Reply