

CCT nayo yatangaza maombi kuwakumbuka waathirika wa Oktoba 29
Dar es Salaam. Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) imetoa wito kwa makanisa wanachama wake, kufanya maombi ya kitaifa kwa walioathiriwa wakati wa vurugu za Oktoba 29, 2025.
Maombi hayo kwa mujibu wa jumuiya hiyo, yajikite katika toba, amani, maridhiano, kadhalika ulinzi wa Mungu dhidi ya maafa yanayoweza kusababishwa na mvua kubwa.
Wito wa jumuiya hiyo, unakuja siku mbili baada ya Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), kutangaza maombi kuwakumbuka waliopoteza maisha wakati wa matukio ya Oktoba 29, 2025.
Taasisi hizo za kidini zinakuja na wito huo, takribani mwaka mmoja tangu matukio ya maandamano yaliyozaa vurugu na kusababisha vifo na uharibifu wa mali, yatokee wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Kwa mujibu wa Tume ya kuchunguza matukio hayo iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande, watu 518 walifariki dunia huku wengine wakijeruhiwa.
Taarifa ya CCT imetolewa Oktoba 23, 2026 na kutiwa saini na Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Mchungaji Stanley Hotay.
Jumuiya hiyo, imewataka viongozi wa makanisa kuongoza waumini kumwomba Mungu awasamehe Watanzania, azifariji familia zilizopoteza wapendwa wao na kuponya majeraha ya walioathirika.
“Tumwombe Mungu atulinde dhidi ya kurudia matukio kama hayo na atujalie amani, haki, umoja na maridhiano ya kweli katika Taifa letu la Tanzania,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
CCT pia imehimiza maombi ya ulinzi wa Mungu dhidi ya mvua kubwa zinazotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ambazo zinaweza kusababisha mafuriko na maafa mbalimbali.
Katika wito huo, jumuiya hiyo imetaka kufanyika maombi ya kuepusha mvua kubwa zinazoweza kuleta uharibifu wa mali, mazao na miundombinu, kusababisha magonjwa na kupoteza maisha.
“Tumwombe Mungu atuepushe na mvua kubwa kupita kiasi na maafa yanayoweza kuambatana na hayo,” imeeleza taarifa hiyo, huku ikihimiza pia maombi ya mvua za wastani zinazofaa kwa kilimo na ustawi wa taifa.
Hata hivyo, CCT imesisitiza umuhimu wa Watanzania kuomba hekima ya kuchukua tahadhari zinazohitajika kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo.
Katika kuhimiza imani na matumaini, jumuiya hiyo imenukuu Isaya 43:2 inayosema: “Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe, na katika mito, haitakugharikisha.”
Wito huo umewaelekeza maaskofu, viongozi wakuu na wakuu wa makanisa wanachama wa CCT kuratibu maombi hayo kupitia ibada, mikutano ya maombi na vikundi vya waumini.“Bwana atutangulie, atulinde na atuongoze katika kipindi hiki,” imeeleza taarifa hiyo.
You may also like

Serikali yatoa kauli tena Sh730 bilioni za El Niño

Rais Samia kuzindua Mji wa Kiserikali Oktoba 30


Leave a Reply