

Rais Samia kuzindua Mji wa Kiserikali Oktoba 30
Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan anatarajia kuzindua Mji wa Serikali wa Mtumba, jijini Dodoma unaojulikana kama Magufuli City, Ijumaa ya Oktoba 30, 2026, katika hatua inayotarajiwa kukamilisha rasmi mchakato wa kuhamishia makao makuu ya Serikali jijini Dodoma.
Awali, uzinduzi huo ulikuwa ufanyike Septemba 8, 2026 na Rais Samia lakini uliahirishwa kufuatia kifo cha mume wa Rais Samia, Ameir Hafidh Hassan, kilichotokea Septemba 7, 2026.
Leo Jumapili, Oktoba 25, 2026, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali, amegusia uzinduzi huo akisema ni hatua muhimu katika utekelezaji wa azma ya Serikali kuhamia Dodoma, miaka 43 tangu uamuzi wa kuhamisha makao makuu ya nchi ulipotangazwa.
Msigwa amesema awamu ya kwanza ya ujenzi wa mji huo imekamilika, huku wizara zote za Serikali zikiwa zimejenga majengo ya ofisi na kuhamia katika eneo hilo, ambako huduma mbalimbali za Serikali zinatolewa.
Amesema majengo ya mji huo yamejengwa kwa viwango vya kisasa ili kukidhi mahitaji ya utoaji wa huduma kwa wananchi. Jengo fupi zaidi lina ghorofa tano, huku mengine yakiwa na ghorofa zaidi.
“Mji huu umejengwa kwa viwango vya kisasa na umezingatia mahitaji ya utoaji wa huduma za Serikali kwa wananchi,” amesema Msigwa.
Ameongeza Mji wa Serikali wa Mtumba umeanza kuwa kivutio cha utalii, huku nchi zaidi ya 10 zikiutembelea kwa lengo la kujifunza na kupata uzoefu wa ujenzi wa miji ya kisasa ya kiutawala kwa ajili ya kuendeleza miradi kama hiyo katika nchi zao.
Kwa mujibu wa Msigwa, ujenzi wa mji huo umegharimu takribani Sh700 bilioni.
Amesema mji huo una mtandao wa barabara za lami wenye urefu wa kilomita 59, pamoja na mifumo ya kisasa ya mawasiliano inayowezesha shughuli za Serikali kufanyika kwa njia za kielektroniki.
Ameeleza kuwa matumizi ya mifumo hiyo yamepunguza utegemezi wa nyaraka za karatasi katika shughuli za kiutawala, hivyo kurahisisha utoaji wa huduma na utekelezaji wa majukumu ya Serikali.
“Kila kitu kinafanyika kwa njia ya kielektroniki. Sikumbuki mara ya mwisho kusaini kwenye makaratasi,” amesema Msigwa.
Amesema mifumo hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuboresha utendaji kazi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Msigwa amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uzinduzi huo utakaofanyika Oktoba 30, akieleza kuwa ni tukio muhimu katika historia ya ujenzi na maendeleo ya Dodoma kama makao makuu ya nchi.
You may also like

Serikali yatoa kauli tena Sh730 bilioni za El Niño

CCT nayo yatangaza maombi kuwakumbuka waathirika wa Oktoba 29


Leave a Reply