

Serikali yatoa kauli tena Sh730 bilioni za El Niño
Dodoma. Serikali imesema Sh730 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya kukabiliana na athari za mvua za El Niño ni jumla ya fedha zilizopangwa na taasisi mbalimbali za umma na binafsi, na si fedha zilizowekwa sehemu moja kama baadhi ya watu wanavyodai.
Imesema fedha hizo zitatumika kukarabati au kujenga upya miundombinu itakayoharibiwa na mvua hizo, ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma muhimu bila usumbufu wa muda mrefu.
Ufafanuzi huo ni wa pili unatolewa takribani mwezi mmoja umepita tangu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba Kabudi alipofafanua bajeti hiyo, baada ya kuibua mijadala maeneo mbalimbali hususan mitandaoni.
Leo, Jumapili, Oktoba 25, 2026, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma naye amegusia suala hilo akisema miundombinu inayolengwa ni pamoja na ya afya, elimu, maji, barabara, madaraja na mawasiliano, ambayo inaweza kuathiriwa na mvua kubwa zinazotarajiwa.
Amesema fedha hizo zitatumika endapo kutatokea maafa au uharibifu, huku kila taasisi ikiwajibika katika eneo lake kwa kushirikiana na Mfuko wa Maafa wa Ofisi ya Waziri Mkuu kurejesha huduma na miundombinu itakayoharibika.
“Fedha hizo zimetengwa na taasisi mbalimbali kwa ajili ya kukabiliana na athari za mvua hizo. Si kwamba zipo sehemu moja, bali kila taasisi imetenga fedha kwa ajili ya eneo lake la uwajibikaji,” amesema Msigwa.
Ameeleza endapo mvua hizo hazitasababisha maafa au uharibifu, fedha hizo zitaendelea kubaki katika taasisi husika na kutumika kwa shughuli nyingine kulingana na mahitaji na taratibu zilizopo.
Msigwa amesema Serikali haiwezi kusubiri maafa yatokee ndipo ianze kutafuta fedha za kukabiliana nayo, hasa baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kutoa utabiri wa mvua hizo.
“Hatuwezi kusubiri hadi madhara yatokee ndipo tutenge fedha. Ni muhimu kuchukua tahadhari mapema ili kuhakikisha huduma muhimu zinaendelea kupatikana hata pale miundombinu itakapoharibika,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, Msigwa amewataka wananchi wanaoishi mabondeni na maeneo yanayopitiwa na maji kuhama kwa muda na kwenda maeneo salama ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na mvua kubwa zinazotarajiwa.
Wananchi hao wametakiwa kuzingatia tahadhari zinazotolewa na mamlaka husika na kutanguliza usalama wa maisha yao na familia zao.
Septemba 2, 2026, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba Kabudi akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma alitaja hatua 12 za kuchukua tahadhari dhidi ya mvua za El Nino, huku ikiwaonya wananchi kutopuuza utabiri huo na kuwataka wanaoishi maeneo ya mabondeni kuanza kuhama mapema.
Miongoni mwa hatua hizo ni kuhakikisha mvua zinatumika vizuri, kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kujiandaa na kupunguza madhara, kutambua maeneo hatarishi, kuimarisha usimamizi wa mazingira na kuweka vifaa vya uokozi katika hali ya utayari.
Profesa Kabudi amesema fedha zilizotengwa moja kwa moja kwa ajili ya majanga na dharura ni Sh10 bilioni, hivyo Serikali imeanza mawasiliano na taasisi na mashirika mbalimbali ili kufikia Sh730 bilioni zitakazohitajika kukabiliana na majanga.
“Siyo kwamba tunazo fedha hizi zote, bali tumeshaanza kuwasiliana na wenzetu wengine na tumeanza kuwaandikia barua mashirika mengine makubwa kupata fedha za kufikia kiwango hicho, ambapo bajeti kamili inahusisha kila mtu na eneo lake,” amesema.
Historia inaonyesha kuwa miongoni mwa vipindi vya El Nino vilivyowahi kusababisha madhara makubwa nchini Tanzania ni mwaka 1950, kikifuatiwa na mwaka 1997.
Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na mamlaka, mvua zinazotarajiwa msimu huu zinatajwa kuwa na kiwango kikubwa zaidi, jambo linalosisitiza umuhimu wa wananchi, Serikali na wadau wengine kuchukua tahadhari mapema.
Serikali imesisitiza kuwa maandalizi ya mapema, ufuatiliaji wa taarifa za hali ya hewa, utambuzi wa maeneo hatarishi na ushirikiano wa wananchi na mamlaka ni muhimu katika kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua hizo.
You may also like

CCT nayo yatangaza maombi kuwakumbuka waathirika wa Oktoba 29

Rais Samia kuzindua Mji wa Kiserikali Oktoba 30


Leave a Reply