

Iran: Mkituchokoza tena tutawatandika vikali, bila kujali mipaka
Iran. Kiongozi Mkuu wa Iran, Mojtaba Khamenei, ameonya nchi yake itapanua wigo wa mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Marekani na Israel iwapo mataifa hayo yataanzisha tena mashambulizi dhidi ya Iran.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari vya kimataifa ikiwamo Fox news, Khamenei ametoa agizo hilo katika mkutano na makamanda wakuu wa kijeshi, akitaka orodha ya shabaha za kijeshi isasishwe ili kujumuisha mali na miundombinu ya Marekani na Israel inayoweza kufikiwa na vikosi vya Iran.
Khamenei amesema aina yoyote ya tishio dhidi ya nchi yake inapaswa kujibiwa mara moja, kwa nguvu na bila kuzingatia mipaka ya kijiografia.
Onyo hilo linaashiria uwezekano wa kuongezeka kwa mvutano wa kijeshi katika Mashariki ya Kati iwapo juhudi za kidiplomasia zitashindwa kuzuia mapigano mapya.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kiongozi huyo amesisitiza kuwa vikosi vya Iran na wananchi wake ndivyo vitakavyoamua muda na masharti ya kumaliza mapigano iwapo mashambulizi yataanzishwa tena.
Onyo hilo linakuja wakati kukiwa na taarifa Rais wa Marekani, Donald Trump, anazingatia uwezekano wa kuanzisha mashambulizi mengine dhidi ya Iran baada ya uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani, unaotarajiwa kufanyika Novemba 3, 2026.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema Trump bado hajafanya uamuzi wa mwisho kuhusu mashambulizi mapya, huku akieleza kuwa Washington inapendelea kutafuta suluhu kupitia diplomasia.
Wakati huohuo, juhudi za kidiplomasia zinaendelea kuzuia kurejea kwa mapigano. Qatar imekuwa ikifanya mazungumzo na maafisa wa Iran, huku Qatar na Pakistan zikishiriki katika juhudi za upatanishi kati ya Tehran na Washington.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema nchi yake imekuwa ikijadili ujumbe uliotumwa na Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, kupitia njia za kidiplomasia. Hata hivyo, amesema kwa sasa hakuna mpango wa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya maoafisa wa Iran na Marekani.
Mvutano huo unaendelea huku kukiwa na hofu kuwa mapigano mapya yanaweza kuathiri zaidi usalama wa eneo hilo na biashara ya kimataifa, hasa katika Mlango-Bahari wa Hormuz, njia muhimu inayotumiwa kusafirisha mafuta kutoka Mashariki ya Kati kwenda masoko ya dunia.
Iran imekuwa ikitishia kupanua wigo wa mapigano iwapo Marekani itaanzisha mashambulizi mengine. Kwa upande mwingine.
Khamenei hajaonekana hadharani tangu alipochukua nafasi ya baba yake, Ayatollah Ali Khamenei, aliyeuawa katika mashambulizi ya Marekani na Israel mwishoni mwa Februari 2026.
Mojtaba alichukua uongozi wa juu wa Iran baada ya kifo cha baba yake, wakati nchi hiyo ikiingia katika kipindi cha mapigano makali na Marekani na Israel.
You may also like

Chadema issues conditions before reconciliation

Joto kali linavyoongeza hatari ya sumu ya chakula


Leave a Reply