

Kahama yakabiliwa na upungufu wa madarasa 246 kabla ya 2028
Kahama. Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga inakabiliwa na upungufu wa vyumba 246 vya madarasa, wakati ikijiandaa kupokea wanafunzi 25,113 wanaotarajiwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2028.
Wanafunzi hao wanatarajiwa kuhitimu darasa la sita na la saba mwaka 2027, hali itakayoongeza mahitaji ya miundombinu ya shule za sekondari katika kata 20 za manispaa hiyo.
Mbali na vyumba vya madarasa, manispaa hiyo inahitaji maabara 26, matundu 536 ya vyoo na samani za shule, zikiwemo viti na meza 16,839, ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi hao.
Takwimu hizo zimetolewa leo, Jumatano, Novemba 25, 2026, na Afisa Elimu Sekondari wa Manispaa ya Kahama, Annastazia Manumbu, katika kikao cha Baraza la Madiwani.
Amesema manispaa hiyo inahitaji jumla ya vyumba 502 vya madarasa, lakini vilivyopo ni 256 pekee, hivyo kuwa na upungufu wa vyumba 246.
Amesema hali hiyo inahitaji ushirikiano kati ya halmashauri, madiwani na wananchi ili kuandaa mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia kabla ya wanafunzi hao kujiunga na sekondari.
“Katika vikao vyetu vya kamati za maendeleo za kata (WDC) vya Julai 2026, tulikutana pamoja na watendaji na kujadiliana nini cha kufanya kukabiliana na changamoto hii. Mahitaji haya ni makubwa, kwa hiyo yanatutaka tushirikiane kuanzia ngazi ya kata,” amesema Manumbu.
Akizungumzia mikakati ya halmashauri, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Masudi Kibetu, amesema baadhi ya kata, zikiwemo Nyahanga, Zongomela na Mhungula, zimeanza ujenzi wa shule mpya za sekondari.
Amesema kata nyingine zimeanza ujenzi wa shule mpya, huku baadhi zikiendeleza maboma yaliyokwishaanza kujengwa.
Amewaomba madiwani kushirikiana na wananchi kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo, akieleza kuwa halmashauri imeweka mpango wa kutumia fedha kutoka Serikali Kuu, mapato ya ndani na wadau mbalimbali.
“Ili kupata madarasa na matundu ya vyoo, tumeweka mgawanyo wa fedha kutoka Serikali Kuu, mapato ya ndani na wadau mbalimbali. Kuna kata zimeshaanza utekelezaji kwenye maeneo yao kama tulivyokubaliana,” amesema Kibetu.
Diwani wa Kata ya Majengo, Zacharia Soko, amesema kwa kushirikiana na wananchi wanatarajia kujenga vyumba vitatu vya madarasa, huku maandalizi ya ujenzi huo yakitarajiwa kuanza Januari 2027.
Amesema tayari wamechukua ramani ya ujenzi kutoka kwa mkurugenzi wa manispaa hiyo.
“Niwahakikishie wananchi wa Majengo kuwa kabla ya 2028 changamoto hii itakuwa imekwisha kwenye kata yangu,” amesema.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Nyahanga, Josephine Kilimba, amesema kata hiyo inatarajia kupokea wanafunzi 5,490 mwaka 2028, huku ikiwa na upungufu wa vyumba 39 vya madarasa.
Amesema wameanzisha ujenzi wa shule mpya ya sekondari na kupanga kujenga vyumba 14 vya madarasa katika hatua za awali kupitia michango ya wananchi.
Amesema tayari wamefanya mikutano na wananchi kuwaeleza umuhimu wa mradi huo, ambao umepokelewa vizuri na jamii, huku uchangiaji ukiendelea.
Kilimba amesema wanatarajia kukamilisha vyumba hivyo 14 ifikapo Juni 2027 ili viweze kusaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa madarasa.
Maandalizi hayo yanakuja baada ya Serikali kuanza kuhimiza halmashauri kujiandaa mapema kwa ongezeko la wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2028.
Agosti 4, 2026, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Uhusiano, Deus Sangu, alizielekeza halmashauri nchini kuanza mapema maandalizi ya miundombinu ya elimu ili kukidhi mahitaji yatakayojitokeza mwaka huo.
Aliwaelekeza viongozi wa halmashauri kuzingatia ongezeko la wanafunzi litakalotokana na wanafunzi wa darasa la sita na la saba kuhitimu kwa pamoja mwaka 2027.
You may also like

Watakaoendesha kwa mwendo kasi kupigwa faini Sh233,000

Nguzo za umeme za Rea zadaiwa kuuzwa hadi Sh300,000 Ushetu


Leave a Reply