

Watakaoendesha kwa mwendo kasi kupigwa faini Sh233,000
Unguja. Madereva watakaobainika kuendesha magari kwa mwendo kasi watatozwa faini ya Sh233, 000, huku wanaotumia bajaji au pikipiki wakitozwa Sh50, 000, Serikali imesema.
Aidha, dereva atakayebainika kuendesha akiwa amelewa baada ya kupimwa atatozwa faini ya Sh116, 500.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Badria Atai Masoud, ametoa viwango hivyo leo Jumatano, Novemba 25, 2026, Barazani alipokuwa akijibu swali la Mwakilishi wa nafasi za wanawake, Fatma Ramadhan Mohamed.
Katika swali lake, Fatma amehoji hatua zinazochukuliwa na Serikali kudhibiti madereva wanaoendesha vyombo vya moto kwa mwendo kasi na wale wanaoendesha wakiwa wamelewa, akisema vitendo hivyo vinahatarisha maisha ya watumiaji wa barabara.
Akijibu, Badria amesema kamera zimefungwa barabarani kwa ajili ya kufuatilia na kubaini makosa hayo.
“Dereva anayepatikana na kosa la mwendo kasi hutozwa faini isiyopungua Sh233, 000 kwa gari na Sh50, 000 kwa bajaji au pikipiki,” amesema.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Badria Atai Masoud, akizungumza leo Jumatano, Novemba 25, 2026, Barazani Chukwani Unguja Zanzibar
Kuhusu madereva wanaoendesha wakiwa wamelewa, amesema anayebainika kuwa na kosa hilo baada ya kupimwa hutozwa faini ya Sh116, 500.
Katika kikao hicho, Mwakilishi wa Malindi, Abdulghani Ismail Zubeir (CCM), ameibua kero ya barabara ya Felix Moumie, Malindi, akihoji sababu za mkandarasi kufukia chemba za maji taka na mitaro na kusababisha usumbufu kwa wakazi wa eneo la Gulioni.
Akijibu hoja hiyo, Badria amesema kupitia Kamati za Malalamiko za Shehia chini ya Mradi wa Kukuza Uchumi Jumuishi Zanzibar (BIG-Z), wizara imekamilisha utambuzi, ufukuaji na marekebisho ya chemba na mitaro iliyokuwa imeziba.
Katika hoja nyingine, Mwakilishi wa Wingwi, Kombo Mwinyi Shehe (ACT Wazalendo), amehoji kama Serikali imefanya tathmini au kukutana na wananchi wa Mjini Wingwi kuhusu athari na taharuki inayosababishwa na uchimbaji wa mawe na kifusi kwa kutumia baruti na mabomu.
Akijibu, Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Seif Kombo Pandu, amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali, ikiwemo kupunguza kina cha uchimbaji hadi mita tatu, kupunguza ulipuaji wa baruti na kuziagiza kampuni kurejesha udongo katika maeneo yaliyochimbwa.
Amesema pia viongozi wa wilaya na wizara wamekutana na wananchi na kukubaliana kuwa kampuni za ujenzi zitumie njia mbadala ili kupunguza matumizi ya baruti.
You may also like

Kahama yakabiliwa na upungufu wa madarasa 246 kabla ya 2028

Nguzo za umeme za Rea zadaiwa kuuzwa hadi Sh300,000 Ushetu


Leave a Reply