

Nguzo za umeme za Rea zadaiwa kuuzwa hadi Sh300,000 Ushetu
Shinyanga. Baadhi ya wafanyakazi wa kampuni zinazotekeleza miradi ya kusambaza umeme vijijini (Rea) katika Halmashauri ya Ushetu, wilayani Kahama, wanadaiwa kuwauzia wananchi nguzo za umeme kwa Sh150,000 hadi Sh300,000 ili waharakishiwe kuunganishiwa huduma hiyo.
Malalamiko hayo yalitolewa na madiwani katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Novemba 25, 2026, wakieleza kuwa vitendo hivyo vinakiuka taratibu za utoaji huduma na maadili ya kazi.
Diwani wa Kata ya Kinamapula, Sharifu Adriano, amesema wananchi wamekuwa wakilalamika kutozwa fedha hizo ili kupata nguzo na kuunganishiwa umeme, badala ya kufuata utaratibu rasmi.
Amesema vitendo hivyo vinadhoofisha jitihada za Serikali za kuhakikisha wananchi wa vijijini wanapata huduma ya umeme kwa gharama nafuu, ili kuboresha maisha na kuchochea shughuli za kiuchumi.
“Tumekuwa tukipokea malalamiko kutoka kwa wananchi wetu. Wamekuwa wakitozwa fedha kuanzia Sh150,000, Sh250,000 hadi Sh300,000 kwa ajili ya kununua nguzo ili wafikishiwe huduma, badala ya kupata huduma hiyo kwa utaratibu unaozingatia gharama zinazopaswa kulipwa,” amesema Adriano.
Akichangia hoja hiyo, Diwani wa Kata ya Igunda, Tabu Katoto, ameiomba mamlaka husika kuchunguza malalamiko hayo na kuchukua hatua dhidi ya wafanyakazi watakaobainika kuwaomba au kuwauzia wananchi nguzo kinyume na utaratibu.
Akijibu malalamiko hayo, Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Halmashauri ya Ushetu, George Madaha, amekiri kuwapo kwa baadhi ya wafanyakazi wasio waadilifu wanaodaiwa kujihusisha na vitendo hivyo.
Ameahidi kufanya ufuatiliaji katika maeneo yanayotekelezwa mradi na kuomba ushirikiano wa viongozi wa maeneo husika ili kubaini wanaokiuka maadili na taratibu za utoaji huduma.
Madaha amesema taarifa kutoka kwa viongozi na wananchi zitasaidia kufuatilia na kudhibiti vitendo hivyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ushetu, Gagi Lala, amewataka madiwani kuongeza usimamizi wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao ili kuhakikisha inatekelezwa kwa kuzingatia malengo yaliyowekwa na kuwanufaisha wananchi.
Amesema madiwani wana wajibu wa kufuatilia miradi katika kata zao na kuwasilisha changamoto zinazojitokeza kwa mamlaka husika ili zipatiwe ufumbuzi.
You may also like

Watakaoendesha kwa mwendo kasi kupigwa faini Sh233,000

Kahama yakabiliwa na upungufu wa madarasa 246 kabla ya 2028


Leave a Reply