

Maisha ya ndoa ni yenu wenza, watoto baadaye
Canada. Kuna ndoa tunaweza kusema si ndoa bali wawili waliowahi kuwa katika ndoa, kwa sababu ya kulazimika kwa sababu mbalimbali.
Leo, tutaelezea ndoa zinazoonekana hai na imara kwa juu lakini zikiwa legelege na mfu kwa ndani.
Katika kudurusu ndoa, tuligundua kuwa kuna wanandoa wanaishi nyumba moja lakini vyumba tofauti. Ukisikia kulazimika na si kupendana ndio huku.
Unakuta wanandoa wana migogoro isiyoisha kiasi cha kutengana. Kuna aina mbili za kutengana. Ya kwanza ni pale wanandoa wanapofarakana hadi kufikia kuamua kila mtu na chumba na hata chungu chake. Aina ya pili ni wale wanaochoka au kuhofia usalama wao na kuamua kuondoka kwenye nyumba yao ya ndoa.
Leo, tutaongelea wale wanaoishi pamoja iwe ni chumba kimoja au vyumba tofauti kwa kulazimika kwa sababu ya watoto. Kimsingi, hawa hawaishi kwa ajili yao bali kwa ajili ya watoto.
Wanaumizana na kukwazana kisa watoto! Mbona watoto wanayo maisha yao wakati ukifika. Mara nyingi, kundi hili huwahusisha wanandoa waliokwisha kuchokana na kushindwa kutatua matatizo yao ambao hawataki watoto wao walelewe na baba au mama wa kambo.
Wengine huamua kwa kulazimika kuendelea kuishi kwenye ndoa ya mateso na migogoro kwa kuchelea kupoteza uhalali wa kumilki mali ambazo wanandoa wanazimilki kwa pamoja.
Pia, wengine hufanya hivyo kwa kuepuka aibu na lawama kutoka kwa jamii ya wanaowazunguka. Hawana haja ya kufanya hivyo. Kwani, hata hao wanaowagopa wanayo matatizo yao tena mengine makubwa na mengi kuliko yao.
Mbali na ujinga, ulazima, hata umaskini, maisha ya aina hii si maisha japo ni aina ya maisha. Maisha ya binadamu ni mafupi sana. Hivyo, ukijua hili, hutakubali kuruhusu maisha yakupige chenga hasa maisha ya ndoa.
Kwa wanaojua namna wanandoa wanavyoweza kutatua matatizo yao na kuacha kulazimika kuishi katika ndoa ya kutengana na mateso ama kwa ajili ya mali au watoto, tunatoa jibu moja kuwa wanandoa wajifunze kuishi kwa ajili yao kwanza na watoto baadaye. Maana, walipokutana na kukubaliana kuingia kwenye ndoa, hawakuwa na watoto.
Isitoshe, hawa watoto wana maisha yao baada ya kufikia umri wa kuweza kujitegemea. Wakati huu ufikapo, wahusika huwa wameshazeeka na kuanza kuishiwa nguvu na saa nyingine hao watoto waliolazimika kuwapigania, wasijue umuhimu na uzito wa jukumu hili kiasi cha kutowasaidia.
Tunasema wazi kuwa ni lazima wanandoa wajifunze namna ya kuyaendea na kuyatatua matatizo yao kwa sababu: Kwanza, hakuna ndoa ya malaika wala watakatifu, bali ya binadamu ambao kukosana ni sehemu ya ubinadamu wao.
Pili, wajue kuwa duniani tunaishi mara moja mbali na maisha yenyewe kuwa na changamoto nyingi na pia tena kuwa mafupi. Wahusika waanze kujifunza kuishi leo na siyo kesho. Tunaamini wakielewa na kuyakubali haya, watatua matatizo yao na kuendelea na maisha yenye furaha kama wengine.
Tatu, isitoshe, wao wanaweza kujiona kama watu wasiofaa na walioshindwa wakati si kweli hasa kama watazingatia kuwa migogoro ni furssa ya kuyajua ambayo hawakuwa hawajui mbali na kuwa sehemu ya kuwezesha akili zao kuwa bunifu nao kuwa wastahimilivu.
Pia, wajue, hakuna wema duniani na kama wapo, na wao ni wema pia sema hawatumii njia bora kutatua matatizo yao. Kimsingi, hao wema na wafaao wasio kama wao hawapo duniani. Hivyo, ni vizuri kukubali ukweli huu na kuanza kufanya na kutafuta mikakati ya kutatua matatizo yenu maana wakosanao ndiyo wapatanao.
Wakati wahusika wakiishi kwa ajili ya watoto, je, huwa wanajiuliza kuwa watoto nao watakuwa tayari kuishi kwa ajili yao watakapokuwa watu wazima? Tukiachana na kukata tamaa na kukosa ubunifu, hivi, kuna tatizo lisilo na suluhu? Japo kutengana kunaweza kuwa suluhisho, ni la muda tu. Ufa ukishaingia, usipozibwa, wahusika watajenga ukuta ambayo ni kazi kubwa kuliko kuuziba.
Kama wanandoa ambao tumeishi kwenye ndoa kwa takribani miaka 30, tumejifunza kitu kimoja kuwa ndoa ni kama mwili wa binadamu. Lazima uhudumiwe iwe kwa kuulisha, kuusafisha, kuutibu, na kuupenda.
Hivyo, wahusika wajue fika kuwa migogoro na ugomvi wao vinaweza kuwa fursa za kujijua, kujuana, na kutafuta namna ya kuvishughulikia. Hivyo, basi, hakuna haja wala ulazima wa kuishi kwa ajili ya wengine kabla ya kuishi kwa ajili yako.
You may also like

Wadau washauri Oktoba 29 iwe siku ya kusaka amani

Moto wateketeza maduka 20 stendi mpya ya Buza Dar


Leave a Reply