

Nyumba 35 zaezuliwa Hanang, DC awatembelea waathirika
Hanang. Nyumba 35 zilizopo mji mdogo wa Katesh, Wilaya ya Hanang mkoani Manyara, zimeezuliwa na upepo mkali baada ya mvua kubwa kunyesha katika eneo hilo.
Nyumba hizo zimeezuliwa jana Oktoba 24, 2026, hivyo kuathiri kaya 35 zilizokuwa zinazoishi katika nyumba hizo.
Mkuu wa wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara, Vita Kawawa akikagua nyumba zilizoezuliwa na upepo mkali baada ya mvua kunyesha mji mdogo wa Katesh. Picha na Joseph Lyimo
Mmoja wa watu walioathirika na janga hilo, John Amsi amesema mvua hiyo ilikuwa kubwa ikiambatana na upepo mkali.
Amsi amesema alikuwa amekaaa ndani ya nyumba wakati mvua inanyesha, ghafla upepo mkali ukaanza kuvuma ukiambatana na ngurumo za radi.
Mkazi mwingine wa eneo hilo, Elizaberth Elibariki amesema wamepata hasara ya nyumba ya familia yao kusombwa na upepo baada ya mvua hiyo kunyesha.
Mkuu wa wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara, Vita Kawawa akizungumza baada ya kukagua nyumba zilizoezuliwa na upepo mkali baada ya mvua kunyesha mji mdogo wa Katesh. Picha na Joseph Lyimo
“Tumesikitishwa na tukio hilo lakini tunamshukuru Mungu hakuna mtu aliyejeruhiwa au kufariki dunia kutokana na mvua hiyo pamoja na nyumba kuezuliwa,” amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Vita Kawawa amekagua uharibifu wa nyumba zilizoezuliwa na upepo kufuatia mvua kubwa iliyonyesha mji mdogo wa Katesh.
Kawawa amewapa pole wananchi walioathirika na tukio hilo, akibainisha kwamba hakuna kifo kilichotokea wala majeruhi.
Amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali.
“Poleni sana wote mliokumbwa na masahibu haya na tuendelee kuchukua tahadhari ya matukio haya ambayo vyombo vya habari vimekuwa vikitangaza kila mara,” amesema Kawawa.
Amewahimiza wananchi kuwa makini, kulinda usalama wa maisha na mali zao pamoja na kutoa taarifa mapema kwa mamlaka husika wanapoona viashiria vya hatari.
You may also like

Wadau washauri Oktoba 29 iwe siku ya kusaka amani

Moto wateketeza maduka 20 stendi mpya ya Buza Dar


Leave a Reply